Wednesday, November 18, 2020

Kamera 306 zafungwa na Serikali kuzunguka ukuta wa madini Mirerani

 


 

Asteria Muhozya na Issa Mtuwa, Mirerani
Kwa mara nyingine tena Ukuta unaozunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani wenye urefu wa kilomita 24.5 umeingia kwenye historia nyingine baada ya kufungwa jumla ya Kamera 306 za Usalama zenye uwezo wa kufanya kazi katika mazingira yoyote ikiwemo kumbaini mhalifu. 
Kamera hizo zimewekwa kufuatia kuwepo umuhimu wa eneo husika kufungwa mfumo wa CCTV kwa lengo la kugundua vitu na watu wanaoingia eneo la Ukuta, kuhifadhi taarifa za Kudumu, kuzuia wanaokusudia kufanya uhalifu na kufuatilia matukio yanayofanyika eneo la ukuta huo.
 
Hayo yalibainishwa Novemba 17, 2020 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila wakati wa Hafla fupi ya kukabidhi mfumo huo kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
 
“Kamera hizi zina uwezo wa kurekodi matukio wakati wa usiku, mchana, wakati wa jua, Kwenye vumbi, wakati wa mvua na zina uwezo wa kumtambua mhalifu aliyekwishafanya uhalifu kwenye Ukuta,’’ alisema Prof. Msanjila.
 
Kufuatia kufungwa kwa mfumo huo, Prof. Msanjila aliwaasa Wafanyakazi wa Wizara ya Madini na Taasisi zilizo chini yake kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku wakisisitiwa kuzingatia Kanuni na Maadili ya Utumishi wa Umma.
 
Aidha, alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa wadau wote katika eneo tengefu la Mirerani kujiepusha na vitendo vya rushwa, utoroshaji wa Madini ama kukiuka Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo mbalimbali inayosimamia Sekta ya Madini na kuiwezesha  Serikali kufikia malengo yake na kuwapo kwa tija katika Uwekezaji mkubwa wa miundombinu uliofanyika hapa Mirerani.
 
Pia, kufuatia matokeo chanya ambayo yanaonekana katika sekta ya madini,Prof. Msanjila alimwakikishia  Rais John Magufuli na watanzania kuwa wizara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali  ndani na nje  itahakikisha kuwa sekta hiyo inadhihirisha kuwa muhimu katika kujenga  wa nchi.
 
Akizungumzia mipango mingine iliyobaki kukamilishwa katika eneo hilo, alisema kwamba ujenzi wa Scanner katika geti kuu la kuingia uko mbioni kujengwa.
 
Akizungumzia mchakato wa zabuni, alisema kabla ya kutangazwa kwa kandarasi hiyo, zipo kampuni zilizojitokeza huku zikianisha gharama kubwa Na kueleza Kampuni ya StarFix iliyoshinda zabuni hiyo ilitumia shilingi bilioni 1.2 kukamilisha kazi husika.
 
‘’Kampuni ya kwanza iliandika andiko la shilingi bilioni 83, la bilioni 76, la tatu bilioni 33, la Nne bilioni 27 lakini huyu mzalendo Kampuni ya Starfix Enterprise ametumia gharama ya Shilingi Bilioni 1.2. Uwekezaji huu wa Serikali kwa pamoja umegharimu takriban kiasi cha shilingi bilioni 4.284,923,915.98,’’ alisema Prof. Msanjila.
 
Akielezea kazi nyingine zilizofanyika katika eneo hilo, Prof. Msanjila alisema Wizara imekamilisha ujenzi wa jengo la Kituo cha Pamoja ndani ya Ukuta, uwekaji miundombinu ya umeme na taa kuzungukia Ukuta umekamilika. 
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu ya Wataalam waliosimamamia kufungwa kwa mradi huo akieleza namna kamera hizo zinavyofanya kazi alisema kuwa, zina uwezo wa kuhakikisha maeneo yote ya ukuta pamoja na maeneo mengine ikiwemo Geti Kuu la kuingilia, chumba cha kuthaminisha madini na vyumba vingine vinaonekana muda wote. Kituo Maalum (CCTV Control Room) cha uangalizi wa mienendo mbalimbali inayooneshwa na kamera zilizofungwa kimekamilika na kuanza kufanya kazi.
 
‘‘Mfumo uliyofungwa una uwezo wa kuonesha maoneo yote vilevile uwezo wa kufanya kazi Kwenye mazingira yote wakati wa mvua, jua Kali, vumbi, hivyo kutoruhusu Tukio lolote kupiga bila kurekodiwa, unauwezo kwa kutoa taaifa mubashara kwa wanaousimamia pindi kuna mtu anaporuka ukuta au matukio yaliyoanishwa kwenye mfumo kama hatarishi,’’ alisisitiza Moshiro.
 
Pia, alieleza kuwa, mfumo huo unao wezo wa kuwabaini wale wote waliokwishafanya matukio ya uhalifu pindi wanapotaka kuingia kwenye lango kuu au wanapotaka kutoka nje ya eneo.
 
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kuejnga Taifa Dkt. Faraji Mnyepe  akipokea Mfumo  huo alisema kuwa,yapo manufaa yanayotokana na kufungwa kwa kamera hizo  ikiwemo kukuza Pato la Taifa kutokana na udhibiti uliokuwa unafanywa wasio waaminifu.
 
Alissitiza kuwa,  wizara hiyo itaimarisha usalama kuzunguka Migodi yote, na kueleza kuwa jukumu la kulinda Usalama usalama ni la wizara hiyo na hivyo kuwahakikishia wachimbaji wote wadogo na Wakubwa usalama.
 
‘’Shahidi wa hili   ni bilionea Saniniu Lazier. Tulimlinda tangu kuzalisha hadi anauza  madini yake. Tunawaomba Wananchi na watanzania wote kulinda Madini Yetu, rasilimali ni jukumu letu wote. Ni malengo yangu wananchi wa Mirerani mtatusaidia kulinda Rasilimali hii,’’ alisema Dkt. Mnyepe.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mhandisi Zephania Chaula alichukua fursa hiyo kuwaalika wawekezaji katika Wilaya hiyo na kuelezea kuwa, mbali tanzanite wizara hiyo imebarikiwa kuwa na madini mengine ikiwemo Green garnet.
 
Mbali na kukabidhiwa kwa mfumo huo, Afisa Mahusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya StarFix  Jason Kyando iliyofunga kamera hizo, alisema kuwa,
 
 
baada ya zoezi la kufunga mfumo kukamilika tulitoa mafunzo kwa wasimamizi wa mfumo huo ambao wote ni vijana wa Kitanzania  walipatiwa mafunzo ya namna ya kusimamia mfumo huo na katika hafla ya jana Watapatiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo.

Tuesday, November 17, 2020

Tanzania Kuuza Tani Milioni Moja Za Mahindi Ya Njano Misri

 


 Wizara ya Kilimo imefanikiwa kupata soko la mahindi ya njano takribani tani milioni moja kwa mwaka nchini Misri kuanzia mwezi Julai mwaka 2021 kupitia kampuni ya Smart Group ya Misri.


Taarifa hiyo imetolewa jana (16.11.2021) jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipoongea na waandishi wa habari ofisini kwake kufuatia kikao alichofanya na Mwenyekiti wa kampuni ya Smart Group ya  nchini Misri Yasser Attia aliyetembelea Tanzania kutafuta masoko ya mazao ya nafaka.


Kusaya alisema Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano na ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Misri umeweza kufanikiwa kuwashawishi wafanyabiashara hao kuja Tanzania kuona na kujadili fursa za masoko ya wakulima ili kuwezesha upatikanaji wa masoko ya mazao.


“Kampuni ya Smart Group toka Misri imekubali kununua mahindi ya njano tani milioni moja toka kwa wakulima wa Tanzania kuanzia mwezi Julai 2021 kufuatia mazungumzo yetu leo hapa Dodoma “alisema Kusaya


Katibu Mkuu Kusaya aliongeza kusema mahindi ya njano yanayotakiwa na kampuni hiyo ni kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha chakula cha mifugo na samaki hali inayotoa fursa kubwa kwa soko la Tanzania kwa kuwa watanzania wengi hawali mahindi ya njano


Kusaya alisema kwa sasa uzalishaji wa mahindi ya njano nchini ni mdogo hatua ambayo itakuwa ni fursa kwa wakulima kuongeza uzalishaji wa mahindi haya.


“Uhalisia uliopo sasa ni kuwa uzalishaji wa mahindi ya njano ni mdogo  kutokana na watanzania wengi kutotumia mahindi haya kama chakula ,hivyo kufuatia makubaliano tutakayoingia na Smart Group tutahamasisha wakulima kuanzia msimu huu Novemba walime kwa wingi kwa kuwa soko limepatikana” alisema Kusaya.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Smart Group ya Misri Yasser Attia alisema nchi inahitaji wa mahindi ya njano takribani tani milioni nane kwa mwaka ambayo kwa sasa zaidi wanaagiza toka Argentina na Ukraine.


Mwenyekiti huyo aliongeza kusema mwelekeo wa serikali ya Misri chini ya Rais Abdel Fattah el-Sisi ni kuona nchi hiyo inawekeza zaidi kwenye mataifa ya Afrika ndio maana wameamua kuja Tanzania kutafuta soko la mazao.


“Tumekuja Tanzania tukiamini ni ndugu zetu tunategemea kuongeza zaidi mahusiano ya kibiashara ili wakulima wa mahindi wazalishe zaidi na kupata faida kupitia ushirikiano huu na Misri “alisema Attia.


Attia aliongeza kusema nchi ya Misri ina uhitaji wa mazao mengi ya kilimo yakiwemo matunda kama parachichi, nanasi, papai, viungo, kahawa, korosho na chai hivyo watatazama ubora na gharama za usafirishaji mazao haya toka Tanzania hadi Misri kwa njia ya bandari ili waingie mikataba ya mashirikiano kwenye biashara.


Kampuni ya Smart Group ya Misri kupitia Mwenyekiti wake Yasser Attia imesema inahitaji mahindi ya njano kwa wingi toka Tanzania ili kutosheleza soko lao kwa ajili utengenezaji vyakula vya mifugo na samaki hivyo kuamua kuja Tanzania  yenye ardhi nzuri na watu wenye kujituma kufanya kazi ikiwemo amani na utulivu.


Ikiwa Tanzania, ujumbe wa kampuni ya Smart Group watatembelea Dodoma, Zanzibar pamoja na Dar es Salaam kujionea na kuzungumza na watendaji wa serikali na sekta binafsi kuhusu ushirikiano wa kibishara kwenye sekta ya kilimo.


Imeelezwa kuwa Tanzania ina mahusiano ya kidiplomasia na nchi ya Misri kwa zaidi ya miaka 56 sasa hali inayopelekea mataifa haya kufanya biashara za kukuza uchumi ambapo Tanzania kupitia maelekezo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati akifungua Bunge la 12 hivi karibuni aliagiza Wizara ya Kilimo kutafuta masoko ya mazao ya wakulima .


“ Rais Dkt.John Pombe Magufuli ameelekeza wizara zetu zitafute masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima, hivyo ujio wa wafanyabiashara toka Misri  ni jitihada za wazi za kuwasaidia wakulima wa Tanzania kukuza uchumi wao na wa taifa jitihada ambazo tutaziendeleza pia kwa mazao mengine tofauti na mahindi ya njano “ alisema Kusaya.

PROF. KIKULA AONGOZA KIKAO CHA TUME YA MADINI

 


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula ameongoza kikao cha kazi cha Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma lengo likiwa ni kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha robo mwaka. 


Kikao hicho kimeshirikisha Makamishna wa Tume ya Madini ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa na mwakilishi kutoka Wizara  ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Daniel Barago.


Makamishna wengine ni pamoja na Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), Haroun Kinega na Dkt. Athanas Macheyeki.


Pia kikao hicho kimeshirikisha viongozi kutoka Tume ya Madini ambao ni pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya, Mkurugenzi wa Huduma za Tume William Mtinya, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki pamoja na maneja na watendaji wengine.


Akizungumza katika kikao hicho Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya ameeleza mafanikio ya Tume ya Madini ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini 38 na vituo vya ununuzi wa madini 39.


Katika hatua nyingine Profesa Manya amesema kuwa ili kuhakikisha watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye Sekta ya Madini Tume ya Madini imekuwa ikitoa elimu kuhusu ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini (local content) ambapo mpaka sasa kampuni za uchimbaji wa madini nchini zimeanza kutangaza fursa kwa ajili ya kutoa huduma kwenye shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini na wananchi kushiriki.


Wakati huohuo kamisheni imeipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli ambapo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2020-2021 imekusanya shilingi bilioni 65.294 sawa na asilimia 125 ya lengo la kipindi husika.

Tuesday, November 10, 2020

TAKWIMU ZAIPAISHA TANZANIA UCHUMI WA KATI -SERIKALI

 


 A

A     Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi (aliyesimama) akitoa ufafanuzi kwenye mkutano wa uelimishajiwa zoezi la ukusanyaji wa takwimu za mifugo,kilimo na uvuvi katika Kijiji cha  Msikii, Kata ya Muhamo, Mkoani Singida hivi karibuni(Pichana John Mapepele).

B

A.      Bibi Salma Mkumbo akiuliza swali kwa wataalamu kwenye mkutano wa uelimishaji wa zoezi la ukusanyaji wa takwimu za mifugo,kilimo na uvuvi katika Kijiji cha  Msikii, Kata yaMuhamo, Mkoani Singida hivi karibuni (Pichana John Mapepele).

c

A.      Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa (aliyesimama) akitoa ufafanuzikwenye mkutano wa uelimishaji wa zoezi la ukusanyaji wa takwimu za mifugo,kilimo na uvuvi katika Kijiji cha  Msikii, Kata yaMuhamo, Mkoani Singida hivi karibuni(Pichana John Mapepele).

DMeneja Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo( aliyesimama) akitoa maelezo kwa  katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi (mwenye miwani) na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa (hayupo pichani) kwenye ofisi ya Serikali ya kijiji cha Msikii, Kata yaMuhamo, MkoaniSingidaHivikaribuni(Pichana John Mapepele).
E
Elibariki Musa, Mkazi wa kijiji cha Msikii Kata ya Muhamo, Mkoani Singida akiuliza swali kwa wataalamu  (Pichana John Mapepele)


Na John Mapepele, Singida 

Serikali imesema takwimu sahihi zilizokusanywa kutoka kwenye sekta mbalimbali za kimkakati za Mifugo, Kilimo na Uvuvi nchini zimeifanya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano Mheshimiwa John Pombe Magufuli kuingia kwenye Nchi za Uchumi wa Kati duniani.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na ujumbe maalum wa kitaifa ulioongozwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi wakati  walipokuwa wanakagua zoezi la kitaifa ya ukusanyaji taarifa za kina za Kilimo, Mifugo, ufugaji wa samaki Mkoani Singida ambalo  limekamilika  hivi karibuni kwa mafanikio makubwa.

“Madhumuni makuu ya Sensa hii ni kupata taarifa muhimu za kilimo, mifugo na uvuvi zitakazotumika katika kupanga na kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya sekta katika taifa la Tanzania, na endapo ukusanywaji wa takwimu utakuwa kwenye ubora unaositahili utasaidia kulifanya taifa kupea kwenye uchumi wa juu kabisa katika kipindi kifupi kijacho” ameongeza Dkt. Chuwa

 

Akifafanua amesema taarifa  kwa mfano za magonjwa ya mifugo na mazao zitaisaidia Serikali kuainisha maeneo yanayokabiliwa na visumbufu/magonjwa  ili kuchukua hatua stahiki na kupanga mipango ya kudhibiti.Pia taarifa kuhusu uzalishaji wa mazao zitasaidia kujua kiasi cha uzalishaji kwa maeneo husika na kuiwezesha Serikali kupanga upatikanaji wa masoko na uwezekano wa kuanzisha viwanda vya kusindika mazao hayo.

 

Aidha amesema taarifa kuhusu upatikanaji na matumizi ya ardhi zitatumika kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi vijijini  hivyo zitatumika kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji hapa nchini.

 

Dkt. Chuwa ameongeza kuwa matokeo ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yanatarajiwa kuweka msingi imara wa sekta hii kwa miaka mingi iyajo, kwa  kuwa Sekta ya Kilimo ina umuhimu mkubwa  kwenye mustakabali wa maisha ya binadamu kwa kuwa ndiyo chanzo cha chakula na malighafi zinazohitajika katika viwanda hususani katika awamu hii inayoongozwa na dira ya uchumi wa viwanda.

 

“Kutokana na umuhimu huo, na kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya Mwaka 2030, Sekta ya Kilimo ilipewa Lengo la Pili  la Kutokomeza Njaa, Kuwa na Uhakika wa Chakula, Lishe Bora na Kukuza Kilimo Endelevu. Aidha, lengo hilo limesisitiza umuhimu wa kuongeza tija katika sekta ya kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao na pia kusisitiza matumizi bora ya ardhi na kurutubisha udongo, ili kuongeza uwezo wa binadamu kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi na athari zake yakiwemo majanga mbalimbali kama mafuriko na ukame pamoja na majanga mengine ikiwemo ndege waharibifu” ameeleza Dkt. Chuwa

   

Dkt. Lutambi amesisitiza kuwa pamoja na faida za jumla ambazo mkulima atakazozipata Sensa hii itamsaidia mtu mmoja mmoja kutatua changamoto mbalimbali katika kilimo,mifugo na uvuvi hasa upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani, upatikanaji wa masoko kwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Ameongeza kuwa takwimu ni kitu cha msingi katika kupanga maendeleo kuanzia kwenye ngazi ya kijiji hadi taifa kwa kuwa zinasaidia kuonyesha changamoto na mafanikio na hivyo kusaidia kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hizo.

“Ni muhimu tukafahamu kuwa takwimu sahihi za mifugo, mazao na uvuvi zitasaidia  uchangiaji wa malighafi za  viwanda  vyetu hivyo kukuza uchumi wetu ambao tunautaka wa viwanda” amesisitiza Dkt. Lutambi

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe, kwenye hotuba yake, wakati  wa ufunguzi wa mafunzo ya wadadisi wa Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/20, iliyofanyika katika Ukumbi wa TMDA,Mwanza Julai, 25 mwaka huu alisisitiza Mwaka huu 2020, Benki ya Dunia imeitangaza Tanzania kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa kipato cha kati, ambapo alisema Taarifa hizi zimeleta faraja kubwa kwa sekta ya kilimo  kwa kuwa ndiyo iliyotoa mchango mkubwa zaidi katika Pato la Taifa wa asilimia 26.6 mwaka 2019 na pia inatoa ajira kwa takribani asilimia 66 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi.

 

“Sekta ya kilimo ilichangia asilimia 24.3 ya mapato ya mauzo nje ya nchi mwaka 2019. Fedha hizi kwa kiasi kikubwa zinatumika nchini katika mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu wezeshi ya barabara, reli, maji, usambazaji umeme na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za jamii kama vile afya na Elimu kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya wananchi” alifafanua Dkt. Bashe

 

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Ripoti ya Tathmini ya Umasikini Tanzania Bara ya Mwaka 2018, sekta hii ikiendelezwa vyema ndio pekee yenye uwezo wa kuleta maendeleo jumuishi nchini, hivyo  kuna umuhimu mkubwa wa zoezi la sensa ya mifugo, mazao na uvuvi likafanyika kwa ubora na kwa umakini  unaositahili.

 

Pia wakati wa tukio la uzinduzi wa mafunzo ya wadadisi wa Sensa hii, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Amina Msengwa amesisitiza kuwa takwimu zina mchango mkubwa katika maandalizi na utekelezaji wa sera na mipango, na vile vile katika kufanya maamuzi sahihi yanayotakiwa kufikiwa kwa kutumia ushahidi stahiki (evidence based decision making).

 Amesema Sensa ya Mwaka wa Kilimo 2019/20, ni ya tano kufanyika hapa nchini tangu nchi ipate uhuru na inafanyika kwenye jumla ya maeneo yaliyochaguliwa ya kuhesabia2,820 ambapo kutokana na maeneo hayo kaya 33,807 kutoka Tanzania bara na Zanzibar.

Kwa upande wake, Meneja Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Singida kwa kusaidia kufanikisha zoezi hili ambalo  limefanyika kwa takribani siku 50 ambapo pia amewapongeza wananchi kwa kutoa ushirikiano wa  kutosha.

 

 Kipuyo amesema taarifa zilizokusanywa kwenye Sensa hii ni za kipindi cha kuanzia tarehe 1 Oktoba, 2019 hadi tarehe 30 Septemba, 2020 na kuongeza kuwa Mkoa wa Singida umekamilisha zoezi hilo kwa maeneo yote ambapo maeneo madogo ya kuhesabia watu yaani Enumaration Areas (EA) 90 yenye kaya 1087 zilizochaguliwa kwa ajili ya kufanyiwa sensa hii zilifikiwa

Monday, November 2, 2020

BODABODA SINGIDA WATOA TAMKO KALI KUELEKEA KUAPISHWA RAIS DKT JOHN MAGUFULI

 

Mwenyekiti wa madereva na wamiliki wa Bajaji na bodaboda Manispaa ya Singida Ahmed Juma akitoa ufafanuzi wa tamko la kulaani vijana wanaotaka kufanya vurugu
Dereva wa Bodaboda Manispaa ya Singida Ramadhani Zuberi akitoka ufafanuzi kwa waandishi ambao hawapo pichani kupinga na kulaani maandamano ya vijana ambao wanataka kutumika kuvuruga amani 
Sehemu ya madereva wa bodaboda Manispaa ya Singida 

John Mapepele na Rose Nyangasa, Singida

Wamiliki na Madereva wote wa Bajaji Mkoa wa Singida wametoa tamko rasmi la kulaani baadhi ya vijana ambao wameanza kutumiwa na baadhi ya vyama vya upinzani kuandamana kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, Mwaka huu.

Akitoa  tamko  kwa  niaba ya wanachama 2000 wa  Mkoa wa Singida  kwenye Kituo cha Bajaji Soko Kuu la Mjini Singida, Mwenyekiti wa Madereva na Wamiliki wa Bajaji na Boda boda Manispaa ya Singida, Ahmed Juma amesema  umoja wao umepinga njama  zinazofanywa na  baadhi ya  vyama  ya kuwatumia madereva  hao na kusisitiza kuwa njama hizo hazitafanikiwa katika Mkoa  wa Singida .

“Tumejipanga kukabiliana na uhuni wowote ambao umepangwa kufanywa kwenye kipindi  hiki na baadhi ya wahuni wachache wasioitakia mema nchi yetu, tunaomba  vyombo vya ulinzi visimamie hili kikamilifu na sisi tupo nyuma yao” aliongeza Juma

Amesema kinachotaka kufanyika sasa baada ya  uchaguzi kukamilika na matokeo kutangazwa  kwa kufuata taratibu zote za uchaguzi na Mamlaka halali ni  vurugu na uvunjifu wa amani jambo ambalo amesema halikubaliki badala yake amewasihi wananchi wafanye kazi  ili  kuiletea nchi yetu maendeleo  zaidi katika awamu ya sasa.

Amemwomba Rais, John Pombe Joseph Magufuli  kuendelea kuiletea maendeleo Tanzania ili itoke kwenye Uchumi wa Kati hadi Uchumi wa juu kabisa  na hatimaye  kuboresha maisha  ya watanzania wote.

Mwenyekiti wa Madereva wa Boda boda  wa  eneo  la Soko Kuu Mjini Singida, Kulwa Moshi ameonya madereva wa Bodaboda ambao kwa namna moja au nyingine  watatumika katika kuvunja Sheria za nchi kwa kupanga  njama za kufanya maandamano  yasiyo ya amani.

Moshi ameongeza kuwa wananchi wameamua kuwachagua viongozi wanao wapenda hivyo hakuna sababu ya watu kuandaa njama za kupinga matokeo ya uchaguzi.

Naye Ramadhani  Zuberi,  Dereva wa  Bajaji kwenye  Kituo Kikuu cha Mabasi  ya Mkoa wa Singida amepongeza Serikali kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu kwa uwazi  ambao umeweza kufuata taratibu zote na kutoa matokoa kwa wakati

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Nchini (NEC), Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli anatarajiwa kuapishwa Novemba 5 Mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

  Na. John Mapepele Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Rufiji. Mhe, Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi nch...