Monday, September 21, 2020

Waziri Zungu Aiteua Benki Ya CRDB Kuwa Balozi Wa Mazingira Katika Uzinduzi Wa Kampeni Ya Pendezesha Tanzania

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu ameiteua Benki ya CRDB kuwa balozi wa mazingira wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Pendezesha Tanzania iliofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari ya Goba, iliyopo Dar es salaam kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).


Akizingumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge, Waziri Zungu aliipongeza Benki ya CRDB kwa utekelezaji wa mikakati ya kusaidia jitihada za Serikali katika kutunza na kuboresha mazingira kupitia kampeni hiyo ya Pendezesha Tanzania ambayo inahamasisha umuhimu wa upandaji miti katika kutunza mazingira.


Waziri Zungu amesema kampeni ya Pendezesha Tanzania imekuja wakati muafaka kwani inaenda sambamba na mkakati wa serikali wa kupanda miti Milioni Moja na Laki Tano kwa kila Halmashauri kwa mwaka ili kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na Kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame.


“Niipongeze Benki ya CRDB kwa ubunifu huu mliokuja nao wa kuwahamasisha watanzania kutunza mazingira yao yaliyowazunguuka. Niwaahidi Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizi ili kwa pamoja tufikie lengo la kuboresha na kuyatunza mazingira yetu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Waziri Zungu huku akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano Benki ya CRDB katika kuweka kipaumbele suala la utunzaji wa mazingira.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuzindua kampeni ya Pendezesha Tanzania katika mkoa wa Dar es Salaam. Kunenge aliwataka wananchi wa mkoa huo kupanda mti mmoja kila mtu katika makazi yao kama sehemu ya kutekeleza kampeni hiyo. “Asanteni sana Benki ya CRDB kwa kutupa heshima wakazi wa Dar es Salaam ya kutupendezeshea jiji letu. Niwaahidi kuwa tutashiriki kikamilifu kuhakikisha tunafikia malengo,” alisema Kunenge.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kampeni hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa sera ya benki hiyo kusaidia shughuli za maendeleo katika jamii ambayo inaelekeza asilimia 1 ya faida kila mwaka kusaidia nyanja za elimu, afya na utunzaji wa mazingira.


“Lengo la kuzindua kampeni hii ni kuendelea kuihamasisha jamii kuona jukumu la kupanda miti ni la jamii nzima. Tumeanza kwa kupanda miti 2000 katika shule zote za msingi na za sekondari zilizo katika Kata ya Goba kwa lengo la kuzifanya shule hizi kuwa na mazingira bora na rafiki kwa watoto kusoma,” alisema Nsekela 

Kampeni ya Pendezesha Tanzania inatarajiwa kufanyika nchi nzima ili kusaidia kuwajengea Watanzania utamaduni wa kupanda na kutunza miti katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. “Tumeanza Dar es Salaam katika shule hizi zilizopo katika kata ya Goba, lakini lengo letu ni kufika katika wilaya na vijiji vyote Tanzania,” aliongezea Nsekela. 

Sambamba na uzinduzi wa kampeni ya Pendezesha Tanzania, Benki ya CRDB pia imetoa msaada wa pampu za maji kwa shule za Sekondari za Fahari, Goba na Kinzudi ili kusaidia kuboresha upatikanaji wa maji katika shule hizo. 


Akizungumza juu mikakati ya biashara inayozingatia mazingira, Nsekela alisema Benki ya CRDB imejiwekea mfumo wa biashara ambao unazingatia utunzaji wa mazingira ikiwamo kuweka sera inayoelekeza utoaji wa mikopo kwa miradi inayozingatia utunzaji wa mazingira, kuanzisha huduma na bidhaa za kidijitali, pamoja na kuwekeza katika mifumo ya ufanyaji kazi inayopunguza matumizi ya karatasi. 

Afisa elimu kata ya Goba, Edward Shilamba aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuanzisha kampeni hiyo ya upandaji miti katika shule za Sekondari na Msingi kata ya Goba. Afisa elimu huyo alimhakikishia Waziri wa Mazingira kuwa wataweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha miti hiyo inastawi kama inavyotarajiwa.

Kutokana na jitihada za kusaidia utunzaji mazingira mpaka, mwaka jana Benki ya CRDB ilikuwa benki ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuweza kutambuliwa na kupata usahili katika Mfuko wa Umoja wa Mataifa unaoshugulikia masuala ya Tabia Nchi “United Nations Green Climate Fund (GCF)”. Kupitia usahili huu, Benki ya CRDB sasa inaweza kushiriki katika kuwezesha miradi mikubwa ambayo ni rafiki wa mazingira, kwa kutoa mikopo ya hadi dola za kimarekani milioni 250 kwa mradi mmoja.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utunzaji mazingira kwa kuhamasisha watanzania kupanda miti ijulikanayo kama “Pendezesha Tanzania" inayoendeshwa na Benki ya CRDB, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jana kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Goba.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utunzaji mazingira kwa kuhamasisha watanzania kupanda miti ijulikanayo kama “Pendezesha Tanzania" inayoendeshwa na Benki ya CRDB, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jana kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Goba.

 


Sunday, September 20, 2020

Serikali Kutokomeza Wadudu Waenezao Magonjwa Ya Mifugo

 


Na. Edward Kondela
Serikali imelenga kukabiliana na magonjwa ya mifugo nchini kupitia taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa kutumia njia ya chanjo pamoja na kutokomeza wadudu wakiwemo mbung’o ambao wanaathiri afya ya wanyama.

Akizungumza katika ziara ya kikazi ya siku moja aliyofanya Mkoani Tanga mwishoni mwa wiki hii, baada ya kutembelea Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka watanzania kutambua kazi kubwa zinafonywa na taasisi za serikali katika kufanya tafiti na kutafuta tiba ya magonjwa ya mifugo nchini.

“Wito wangu kwa wafugaji ambao bado wanasumbuliwa na mbung’o, tayari kituo chetu cha TVLA Mkoani Tanga wameshapata njia nzuri na rahisi kabisa, lengo kubwa kabisa ni kuhakikisha tunatokomeza magonjwa ya mifugo kadri inavyowezekana, niombe watanzania watambue kazi kubwa zinazofanywa na taasisi zetu, ili tuondoke katika ufugaji wa mazoea bali sasa tufanye ufugaji wa kisayansi.”  Amesema Prof. Gabriel

Afisa Utafiti wa Mifugo kutoka TVLA Mkoani Tanga Bw. Peter Lucas, amemfahamisha Prof. Gabriel kuhusu njia rahisi ambazo wafugaji wanaweza kutumia katika kutokomeza mbung’o kuwa ni pamoja na mtego wa kukamata mbung’o na njia ya kuweka dawa maalum ya kuua mbung’o kwenye vitambaa vyenye rangi ya bluu na nyeusi ambazo zimekuwa zikiwavutia wadudu hao.

Akiwa katika chuo cha Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Kampasi ya Buhuri Mkoani Tanga, Katibu Mkuu Prof. Gabriel amewataka wakufunzi wa chuo hicho wawe na upeo mkubwa ili waweze kutoa wahitimu waliopata elimu bora.

“Kikubwa wafundisheni wanafunzi kujiajiri na anayefundisha somo hilo lazima awe amejiajiri, lazima tuwajengee wanafunzi wetu kazi siyo mpaka kuajiriwa, kujiajiri pia ndiyo msingi hasa wa kuendeleza maendeleo na nchi zilizoendelea walioleta maendeleo ni wajasiriamali.” Amefafanua Prof. Gabriel.

Katika ziara hiyo ya siku moja Mkoani Tanga, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel alijionea shughuli zinazofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) mkoani humo, ambapo ameitaka taasisi hiyo kutoa taarifa ya tafiti mbalimbali za mifugo ikiwemo ya ng’ombe bora wa maziwa na kuongeza idadi ya mifugo iliyopo katika eneo hilo.

Aidha, akizungumza na watumishi wa taasisi hizo Prof. Gabriel amewataka watumishi hao kuwa wazalendo na kujituma kwa kutoa michango yenye tija katika taasisi wanazofanyia kazi.

Wakizungumza katika nyakati tofauti Kaimu Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Oliva Manangwa amemuarifu katibu mkuu huyo kuwa TVLA imefanikiwa kufanya tafiti mbalimbali ikiwemo ya kutokomeza kabisa vimelea vya ndorobo visiwani Zanzibar kwa kuwahasi mbung’o dume.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Mkoa wa Tanga Dkt. Zabron Nziku amemweleza Katibu Mkuu Prof. Gabriel kuwa wameanzisha maabara ya kisasa kwa ajili ya kutengeneza virutubisho vya mifugo vinavyotokana na zao la muhogo ambavyo havina gharama kubwa kwa wafugaji.

Naye Meneja wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Kampasi ya Buhuri Mkoani Tanga Bw. Venance Tarimo amesema chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ili kupata wataalam bora wa mifugo nchini.

Akihitimisha ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Tanga katika taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Bi. Judica Omari na kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazowakumba wafugaji katika mkoa huo na namna ya kuzitatua.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Tanga mwishoni mwa wiki hii ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) ambazo zote zipo chini ya wizara hiyo.

Friday, September 18, 2020

TANZANIA INA CHAKULA CHA KUTOSHA-KM KUSAYA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akizungumza wakati alipofungua kongamano la pili la Kitaifa la Kuzuia Upotevu wa Mazao Baada ya Mavuno mjini Morogoro leo

Bw.Felix Bachmann Mkurugenzi Mkazi wa shirika la HELVETAS nchini akizungumza wakati wa kongamano la pili la Kuzuia Upotevu wa mazao ambapo  amesisitiza matumizi ya teknolijia zitakazopunguza matumizi ya kemikali kwenye uhifadhi wa mazao .

Sehemu ya washiriki wa   kongamano la pili la Kitaifa la Kuzuia Upotevu wa Mazao Baada ya Mavuno linalofanyika chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Morogoro.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wadau wa Kilimo Wasio wa Kiserikali (ANSAF) Audax Rukonge akizungumza kwenye kongamano la kitaifa la kuzuia upotevu wa mazao ambapo ameiomba seriklai kuweka mazingira wezshi kwa viwanda  vingi kuanzishwa ili kuchakata mazao yatakayosaidia kupunguza hasara ya upotevu kwa wakulima.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Prof.Raphael Chibunda amsema upotevu wa mazao katika nchi za kiafrika ni mwendelezo wa matatizo ambayo waliotutawala walituachia na sasa hatujapata suluhisho hivyo ametoa wito kwa watafiti kujikita kutafuta suluhisho hususan kwenye vyuo vikuu nchini.

*******************************

Serikali imesema wananchi waendelee kufanya kazi zao bila hofu kwa kuwa nchi ina chakula cha kutosha licha ya kuwa na uwezekano wa kutokea mvua kidogo msimu ujao.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya leo (18.09.2020) wakati alipofungua kongamano la pili la Kitaifa la Kuzuia Upotevu wa Mazao baada ya Mavuno linalofanyika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Morogoro.

Tunacho chakula cha kutosha hata endapo mvua ikipungua kwa misimu ujao , serikali imejipanga kukabiliana na upungufu huo hivyo wananchi endeleleni kufanya kazi kwa bidii na kutunza chakula mlichonacho.

“Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imejipanga vizuri katika kuhakikisha kuwa maeneo hayo, yanakuwa na chakula kwenye masoko yao. Nitoe rai kwa watanzania kutumia vizuri chakula kilichopo ili kuondoa upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza” alisema Kusaya.

Katibu Mkuu huyo alisema uzalishaji wa chakula nchini Tanzania, unatosheleza mahitaji ya taifa na kuwa hali ya chakula mwaka huu ni nzuri, kutokana na uzalishaji mzuri katika msimu wa 2019/2020.

Kusaya aliendelea kusema tathmini iliyofanyika hivi karibuni ya msimu wa 2019/2020, inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula unatarajia kufikia tani 17,742,388 ambapo mahitaji ni tani 14, 347,955.

“Nchi inategemewa kuwa na ziada ya tani 3, 511,620 za chakula ambapo tani 1, 322,020 ni za mazao ya nafaka na tani 2, 072,413 ni za mazao yasiyo nafaka” alisitiza Kusaya.

Jitihada nyingine za serikali katika kuhakikisha nchi inakuwa na chakula za kutosha ni kuendelea kununua mazao ya nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ambapo tayari tani 100,000 za mazao zimekwisha nunuliwa ikiwemo mahindi na mpunga.

Kuhusu suala la upotevu wa mazao Wizara ya Kilimo imewashukuru wadau wa sekta ya kilimo kwa kuandaa kongamano hilo ili kujadili mikakati ya kudhibiti wa upotevu wa mazao baada ya mavuno ambao unaathiri uchumi wa wakulima, alisema Kusaya.

Akizungumzia hali ya upotevu wa mazao baada ya mavuno nchini,Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Kitaifa la Kusimamia Udhibiti wa Mazao wanaosimamia mazao baada ya Mavuno (TPMP) Julius Wambura alisema takwimu zinaonesha asilimia 30 hadi 35 ya mazao ya nafaka hupotea wakati wa mavuno na baada ya kuvunwa shambani.

“ Jumla ya gunia 3 hadi 3.5 kati ya 10 zinapovunwa zinapotea shambani au baada ya kufikishwa ghalani hali inayowatia umasikini wa kipato wakulima wetu na kuwapunguzia tija” alisema Wambura.

Aidha alitoa wito kwa wadau wa kilimo kutafuta mbinu na teknolojia rahisi kuwasaidia wakulima kutoendelea kupoteza mazao yao ili kuwa na uhakika wa chakula na kipato.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Prof.Raphael Chibunda alisema upotevu wa mazao katika nchi za kiafrika ni mwendelezo wa matatizo ambayo waliotutawala walituachia na sasa hatujapata suluhisho .

Alikemea tabia wa watafiti wakiwemo kwenye vyuo vikuu kutofanya tafiti za kusaidia wakulima kuondokana na tatizo la upotevu wa mazao kwani vyuo vingi havifundishi wanafunzi kukabiliana na tatizo hilo

“ Tunafanya tafiti nyingi lakini haziendi kutatua kero za upotevu wa mazao shambani.Nchi hii inakula ugali lakini hakuna maprofesa wa ugali,wengi waliopo wamebobea kwenye biskuti “alisema Prof.Chibunda.

Prof.Chibunda alitoa wito kwa mamlaka za udhibiti kama TMDA,TBS,Polisi kusaidia wakulima nchini kuwa na uhakika wa kusafirisha mazao yao na kupunguza vikwazo kwa wakulima ili mazao yasiharibike kabla hayajafika sokoni au ghalani.

Akizungumza kwa niaba ya wadau wa kilimo,Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wadau wa Kilimo Wasio wa Kiserikali (ANSAF) Audax Rukonge alisema anaiomba serikali iendelee kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa teknolojia rahisi ya kuchakata na kuhifadhi mazao ili wakulima wapate faida hali itakayosaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.

Kongamano hili linafanyika mara ya pili kwa lengo la kujadili mikakati ya kusaidia kudhibiti upotevu wa mazao baada ya mavuno ambapo lilikuwa lifanyike mwezi Februari mwaka huu lakini likaahirishwa kutokana na janga la korona.

Aidha kongamano hili ni matokea ya uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao Baada ya Kuvuna (2019-2029)ulizinduliwa Agosti 2019 na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima Nane nane, iliyofanyika mkoani Simiyu.

Tuesday, September 15, 2020

SERIKALI YAZIDI KUWEKA MIKAKATI ILI WAFUGAJI WAWE NA NG’OMBE BORA.

 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyevaa miwani) akiwaongoza wafugaji wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kuzindua zoezi la uhimilishaji (kupandikiza ng’ombe mimba kwa njia ya mrija).

Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael akizungumzia kambi ya uhimilishaji katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya na namna wizara inayoshirikiana na wananchi ili kuhakikisha wanapata mifugo bora.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Bi. Rahabu Galahenga ambaye amehitimu diploma ya sheria. Prof. Gabriel amefika katika Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kwa ajili ya kuzindua kambi ya uhimilishaji.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama katikati), akiwa na wasichana wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya waliohitimu masomo kutoka vyuo mbalimbali nchini. Kutoka kulia ni Bi. Naishiye Eliakimu amehitimu shahada ya ualimu, Bi. Naumu Silomi amehitimu diploma ya uhandisi wa ndege, Bi. Rahabu Galahenga amehitimu diploma ya sheria na Bi. Hawa Julius amehitimu diploma ya ualimu.Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akimpongeza mfugaji wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, baada ya ng’ombe wake kufanyiwa vipimo kwa ajili ya kufanyiwa uhimilishaji.

********************************

Na. Edward Kondela

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amesema serikali imelenga kuhakikisha wafugaji nchini wanakuwa na ng’ombe bora, wenye kutoa nyama bora na maziwa mengi wanaopatikana kwa njia ya uhimilishaji (kumpatia ng’ombe mimba kwa njia ya mrija).

Prof. Gabriel amesema hayo katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakati akizindua rasmi kambi ya uhimilishaji katika kijiji hicho kwa wafugaji wa jamii ya kimasai na kuwataka waache kufuga kwa mazoea bali wawe na ng’ombe bora na wenye tija huku akiwalenga zaidi akinamama nchini kujikita katika ufugaji wa kisasa.

“Haya ni mafanikio makubwa niwaombe akinamama wengine Tanzania waige mfano wa kina mama wenzano wa jamii ya kimasai walioamua kufuga kisasa kwa kuwa na ng’ombe bora hatuwezi kuendelea kwenye ufugaji wa zamani lazima tufuge kisasa na uhimilishaji unafanyika kwa ng’ombe yeyote hata wa kienyeji.” Amesema Prof. Gabriel

Prof. Gabriel akizungumzia faida za uhimilishaji amesema njia hiyo ya kumpatia ng’ombe mimba kwa njia ya mrija ni muhimu katika kuendeleza ubora wa mifugo hiyo ili kutengenzea mbari na kosaafu bora ya ng’ombe.

Amefafanua kuwa uhimilishaji ni muhimu kwa kuwa mfugaji anaweza kuchagua ng’ombe anayemtaka na ubora wake pamoja na kudhibiti magonjwa ya mifugo hiyo kwa ng’ombe dume kupanda ng’ombe wengi kwa wakati mmoja.

Ili kutoa hamasa kwa wafugaji wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Katibu Mkuu Wizara Mifugo na Uvuvi amesema wafugaji watakaohimilisha ng’ombe elfu moja wa mwanzo wizara itagharamia kama sehemu ya uzinduzi na uimarishaji wa kambi za uhimilishaji.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo Bw. Stephen Michael amesema wizara imekuwa ikifanya kazi karibu na wananchi hali iliyofikia kuweka kambi ya uhimilishaji katika Kijiji cha Matebete na kuwafanyia ng’ombe vipimo kabla ya kupandikizwa mbegu.

Naye Afisa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Fadhil Chamwazi ameongeza kuwa kambi za uhimilishaji zina malengo ya kuhamasisha wafugaji kutumia huduma ya uhimilishaji na kuwajengea uwezo jamii ya wafugaji na wataalam juu ya faida ya uhimilishaji.

Bw. Chamwazi amesema zoezi hilo limeanza katika mwaka wa fedha 2019/20 na kwa mwaka 2020/2021 limezinduliwa mkoani Tabora na sasa katika Mkoa wa Mbeya katika Kijiji cha Matebete na kubainisha kuwa vigezo vinavyoangaliwa kwa ng’ombe kabla ya kupandikizwa mbegu ya uzazi kwa njia ya mrija, wataalamu wanakagua afya ya ng’ombe pamoja na kuzingatia umri na muonekano wake.

Nao baadhi ya wafugaji wa jamii ya kimasai katika kijiji hicho wamefurahishwa na zoezi hilo na kuiomba serikali kuendelea kuwapatia elimu zaidi na kuwafahamisha namna bora zaidi za ufugaji wa ng’ombe bora wa kisasa ili waweze kupata matokeo chanya katika ufugaji wao.

RC TABORA AAGIZA WAFANYABIASHARA KULIPA KODI KWA WAKATI ILI KUEPUKA FAINI

 

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo ambayo imelenga kusikiliza maoni ya walipakodi, kuwakumbusha kulipa kodi kwa wakati, kusikiliza changamoto walizonazo na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi. Kampeni hiyo itamalizika tarehe 19 Septemba, 2020. Kushoto ni Meneja wa TRA Mkoa wa Tabora Thomas Masese na kulia ni Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi Diana Masalla.

Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi Diana Masalla akizungumza na waandishi wa habari kuhusu idadi ya wafanyabiashara waliokusudiwa kufikiwa na kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani Tabora. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati na Kushoto ni Meneja wa TRA Mkoa wa Tabora Thomas Masese.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tabora Thomas Masese akizungumzia makusanyo katika mkoa huo wakati wa mkutano wa waandishi wa habari kuhusu kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo. Kulia ni Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi Diana Masalla na kushoto ni Afisa Msimamizi wa Kodi Geofrey Comoro.

Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakielekea katika maduka ya wafanyabiashara mkoani Tabora kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo. Kampeni hiyo itamalizika tarehe 19 Septemba, 2020.

Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakimuelimisha mfanyabishara wa maeneo ya soko kuu mkoani Tabora wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo. Kampeni hiyo itamalizika tarehe 19 Septemba, 2020.

Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakimuelimisha mfanyabishara wa maeneo ya soko kuu mkoani Tabora wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo. Kampeni hiyo itamalizika tarehe 19 Septemba, 2020.

 

 Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora

…………………………………………………………….

 NA MWANDISHI WETU,

MKUU wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati ametoa wito kwa wafanyabiashara,wananchi kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka usumbufu na faini ambayo wanaweza kutozwa kwa wale wanaochelewa.

Alitoa kauli hiyo leo kwenye kikao cha waandishi wa habari na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati akizungumzia kampeni inayoendelea mkoani hapa ya elimu kwa mlipakodi inayojulikana kama mlango kwa mlango.

Dkt. Sengati alisema kuwa kodi ndio inayoiwezesha Serikali kugharamia huduma za jamii ikiwemo kujenga vituo vya afya na kuboresha barabara na madaraja, utoaji elimu bure ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara ya watumishi wa umma.

Aliwataka wafanyabiashara mkoani Tabora kutoa ushirikiano kwa Maafisa wa TRA watakaopita katika shughuli zao za biashara wakifanya zoezi hilo la kutoa elimu ya kodi.

“Ninawaasa wafanyabiashara na walipakodi wote mkoani hapa kutoa ushirikiano kwa maafisa wa TRA na watumie elimu hiyo kama fursa ya kupata uelewa na kutoa maoni yao kwa ajili ya maboresho ya Sheria za Kodi”, alisema Dkt. Sengati.

Alisema kuwa Mamlaka ya Mapato imeamua kutoa elimu hiyo ili walipakodi wapende kulipa kodi kwa hiari na isionekane wanashinikizwa bali waone ni haki yao kufanya hivyo.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote ambao watakutwa wakiuza bidhaa zao bila kutoa stakabadhi zinazotolewa kwa njia ya mashine za kieletroniki (EFD).

Naye Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Makao Makuu Diana Masalla alisema kuwa lengo la kampeni hiyo ni  kusikiliza maoni ya walipakodi kwa ajili ya kuboresha huduma za TRA na kuongeza walipakodi wapya.

Alisema kuwa wakati wa utoaji elimu hiyo watawakumbusha wananchi kulipa kodi stahiki na kwa wakati, kusikiliza kero na changamoto walizonazo na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi.

Masalla alitaja maeneo ambayo wanakusudia kutembelea katika zoezi hilo la utoaji elimu kwa wafanyabiashara kuwa ni ni pamoja na  soko kuu la  Manispaa ya Tabora, Nzega mjini Igunga,  Choma, Nkinga na Simbo.

Alisema lengo ni kuwafikia wafanyabiashara 3,500 katika kipindi cha wiki moja watakayokuwa wakitoa elimu ya mlipakodi mkoani Tabora.

Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka Makao Makuu Dar es Salaam wakishirikiana na Maafisa wa TRA wa Mkoa wa Tabora wameanza kampeni ya elimu kwa mlipakodi iliyopewa jina la ‘’Mlango kwa mlango’’.

Kwa Mkoa wa Tabora, Kampeni hiyo imeanza tarehe 14 na itamalizika tarehe 19 Septemba, 202

Thursday, September 10, 2020

TPDC YABAINI UWEPO WA VIASHIRIA VYA MAFUTA BONDE LA MTO MANONGA

 

Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela akiongoza ujumbe wa Mkoa wa Shinyanga kutoa maoni kwa wataalam wa TPDC walofika ofisini kwake kutambulisha mradi wa utafiti wa Mafuta katika Bonde la mto Manonga eneo la Kishapu Mkoani Shinyanga. 
Baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Shinyanga wakifuatilia kwa makini ujumbe wa wataalam wa TPDC waliofika Mkoani Shinyanga kwa kalengo la kutambulisha mradi wa utafiti wa awali kuhusu utafutaji wa mafuta katika Bonde la Mto Manonga Wilaya Kishapu Shinyanga.


Baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Shinyanga wakifuatilia kwa makini ujumbe wa wataalam wa TPDC waliofika Mkoani Shinyanga kwa kalengo la kutambulisha mradi wa utafiti wa awali kuhusu utafutaji wa mafuta katika Bonde la Mto Manonga Wilaya Kishapu Shinyanga.

…………………………………………………………………………….

Na Mwandishi wetu Shinyanga.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi wa utafutaji wa mafuta katika bonde la mto Manonga baada ya utafiti wa awali kubaini uwepo wa miamba yenye viashiria vya mafuta katika bonde la mto huo.

Mradi huo ujalikanao kama EYASI –WEMBELE unatatekelezwa katika Mikoa ambayo mto huo unapitia ikiwemo bonde la Ziwa EYASI na bonde la mto Manonga unaopatikana katika Mikoa ya Tabora, Shinyanga, Singida na Manyara.

Akitambulisha Mradi huo kwa uongozi wa Mkoa wa Shinyanga jana Mtaalam Mshauri wa Mradi huo Dkt. Allan Mzengi kutoka TPDC alisema Mradi huo unaanza na hatua ya awali ya kuangalia athari za kimazingira katika Wilaya Kishapu Mkoani Shinyanga hatua itakayoshirikisha wadau kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kata.

Dr. Mzengi aliuambia uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kuwa pamoja na kuangazia suala la kimazingira hatua ya pili ya mradi itakuwa ni ujenzi wa Mkuza katika eneo ambao mradi huo utatekelezwa na baadae kuweka vilipuzi vitakavyosaidia kubaini maeneo ya ujenzi wa visima vya majaribio ya utafutaji mafuta katika eneo la mradi.

Aidha Mjilojia Kutoka TPDC Bw. Gaston Canuty aliuambia uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kuwa tayari TBDC imeishachimba visima vifupi katika eneo la mradi kubaini miamba yenye uwezekano wa kuifadhi mafuta na sasa mradi huo unakusudia kwenda mbali zaidi kuangalia mafuta yako wapi chini ya Ardhi baada ya kubaini miamba hiyo katika eneo la Kishapu.

Ili kufanikisha zoezi hili Bw. Gaston aliongeza kuwa utafiti utatumia njia ya jiofizikia ambapo watajenga mikuza ambayo itawekwa vilipuzi laini ambavyo vitakapolipuliwa vitawawezesha kupata data chini ya ardhi itakayowawezesha kutambua mahali penye uwezekano wa mafuta.

Bi. Loveness Njogela ambaye pia ni Mjiolojia alisema utafiti wa Mafuta katika eneo la Mradi ulianza kwa tumia ndege ya utafiti ambayo iliwawezesha kuona maeneo yenye miamba yenye tabaka gumu na ile ya tabaka laini na kwa kanuni za kijiolojioa maeneo yale ambayo yana mkandamizo mkubwa wa miamba tabaka ndiyo yatakayofanyiwa jaribio la utafutaji mafuta.

Bi. Njogela aliongeza kuwa pamoja na baadhi ya maeneo kuwa na miamba yenye mgandamizo mkubwa inayotumika kama sampuli mafuta yana tabia kuama katika eneo la miamba hiyo na kutafuta mtego mahali pengine ndio maana wataweka vilipuzi laini vitakavyowezesha kutambua ni wapi kuna uwezekano wa kuwa na mtego wenye mafuta.

Wakati huo Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela alihaidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalam hao kwa lengo la kufanikisha utafiti huo ambao utafanyika katika kata za Mwamalasa, Gana na Mwamashele Wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga.

WAAJIRIWA WATAKIWA KUWASILISHA TIN NAMBA KWA WAAJIRI WAO

 




Mkurugenzi wa elimu kwa mlipa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)leo  jijini Dar es Salaam leo.

Na Ripota wetu, Michuzi TV

MAMLAKA ya mapato Tanzania (TRA) imewataka waajiriwa wote ambao wanalipwa mshahara kwa payroll  kuwa na TIN namba na kuziwasilisha kwa waajiri wao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam leo, Mkurugenzi wa elimu kwa mlipa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA,) Richard Kayombo amesema kuwa kuanzia mchakato hua umeanza mwezi Agosti, 2020 na mwisho wa kuwasilisha TIN hizo ni Desemba 31, 2020.

 "Mtumishi ambaye ameajiriwa popote pale anatakiwa kupata TIN namba na kuiwasilisha kwa mwajiri wake." Amesema Kayombo.

Hata hivyo amesema kuwa  mwajiriwa ambaye amepoteza TIN namba au hana afike ofisi za TRA ili aweze kupata TIN nyingine na kwa ambaye hana kabisa atembelee tovuti ya TRA ili aweze kuipata.
 
"Zoezi hili ni la watumishi walioajiriwa popote pale wawasilishe TIN kwa mwajiri litadumu hadi Desemba 31,2020, kwahiyo waajiri wote tumeshawaagiza wahakikishe wafanyakazi wao wamewasilisha TIN zao."

Na kwa mwajiriwa ambaye  hakuweza kupeleka TIN Kwa mwaajiri wake hataweza kupata mshahara ifikapo Januari mosi, 2021.

Kayombo amesema kuwa hakuna haja ya kuongeza muda kwa kuwasilisha TIN au kodi za mshahara kwa sababu TIN hizo zinawasikishwa kwa njia ya mtandao popote mtu alipo anaweza kuwasilisha.

"Kwa kipindi hiki tumerahisisha kwa kila mtu kutumia mtandao ili kuondoa usumbufu kwa mtu yeyote kufika ofisi za TRA." Amesema Kayombo.

Hata hivyo Kayombo amesema kuwa kampeni ya Mlango kwa Mlango imeendelea kuwafikia watu wengi zaidi.

Amesema kampeni ya Mlango kwa mlango kwa Septemba watafanyia kazi katika mikoa michache ambayo ni Arusha, Mtwara, Kagera Tabora na Mkoa wa Dar es Salaam watafanyia kazi katika wilaya ya Ubungo.

Amesema Kampeni ya Mlango kwa Mlango ni mahususi kuwafikia walipa kodi katika biashara zao na kutomsumbua mfanyabiashara kufika katika Ofisi za TRA.

Wednesday, September 9, 2020

TRA YAENDESHA ZOEZI LA ELIMU KWA MLIPAKODI ARUSHA

 Mkuu wa Mkoa wa Ausha akizindua rasmi Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi iliyoanza rasmi tar.7sep2020 mkoa wa Arusha lengo likiwa ni kujenga ukaribu kati ya TRA na wafanyabiashara.Afisa msimamizi kodi mkuu James Ntalika kutoka kitengo cha Elimu kwa mlipakodi TRA makao makuu Dar es Salaam,na Eugeni Mkubo kutoka TRA Arusha wakitoa elimu kwa wafanyabiashara katika maeneo ya stendi ndogo mkoani hapa. Robert Tarimo mfanyabiashara wa duka na.360 ameishauri TRA mara baada ya kupatiwa elimu ya mkipakodi kwamba kabla ya kuwakadiria kodi ni vyema wakawatembelea ili waweze kuwakadiria kutokana na biashara zao Afisa msimamizi kodi mkuu James Ntalika kutoka kitengo cha Elimu kwa mlipakodi TRA makao makuu Dar es Salaam,akitoa elimu ya mlipakodi kwa mfanyabiashara Alphonce Chaki katika eneo la stendi ndogo iliyopo Jijini Arusha.Afisa TRA kutoka makao makuu Jijini Dar es salaam Juliety Kidemi akiendelea kutoa elimu ya mlipakodi kwa mfanyabiashara mwenye duka no 266 Maria Hassan Matoto.Afisa TRA kutoka makao makuu Jijini Dar es salaam Mercy Macha akiendelea kutoa elimu ya mlipakodi kwa mfanyabiashara mwenye duka no 132 maeneo ya stend ndogo Jijini Arusha .


TRA YAENDESHA ZOEZI LA ELIMU KWA MLIPAKODI ARUSHA

Na.Vero Ignatus.

Mamalaka ya mapato imeendesha kampeni ya elimu kwa mlipa kodi kwa muda wa wiki moja katika mkoa wa Ausha dhumuni kubwa likiwa ni kuhamasisha umma katika uelewa wa masuala ya kodi ili waweze kutimiza wajibu wao kisheria wa kulipa kodi 

Akizindua kampeni hiyo mkuu wa mkoa wa Arusha Idd Kimanta, amewasisitiza TRA wahakikishe kwamba ,kampeni hiyo ya elimu kwa mlipakodi inafanyika katika mkoa wote ,na wasikazanie mjini tu bali waende katika wilaya zote 6 ndani ya mkoa,sekta zote,zikiwemo za utalii ,kilimo ,ufugaji,na wafanyabiashara wa aina zote na wananchi wote wanaopaswa kulipa kodi. 

Alisema kuwa kodi ya mapato inamanufaa makubwa kwa nchi ,ambapo miradi mbalimbali imekuwa ikitekelezwa na serikali,amesema miradi mikubwa ya kimkakati na ile ya kimaendeleo, inayosimamiwa na serikali kwa maelekezo ya Rais Magufuli inatokana na kodi zinazolipwa

''Miradi hiyo ni kama bwawa la umeme la Mwl.Nyerere,Treni ya mwendokasi,ununuzi wa ndege kubwa za abiria ,ujenzi wa miundombinu ya barabara kama vile fly overs za kuunganisha mikoa na ''Kimata

Kimanta alisema ukusanyaji wa kodi unafanyika nchi nzima kupitia TRA,ambapo mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika makusanyo ya kodi, licha ya changamoto mbalimbali ,katika kipindi cha mwaka uliopita 2019/20 walikusanya jumla ya shilingi Bil.420.83 ikiwa ni ongezeko la 12% ukilinganisha na kipindi kama hiki kwa mwaka wa fedha uliopita.

Akizungumza Afisa msimamizi kodi mkuu James Ntalika kutoka kitengo cha Elimu kwa mlipakodi TRA makao makuu Dar es Salaam,anasema lengo lao ni kuweka ukaribu kati yao na wafanyabiashara ambapo zoezi hilo ni la nchi nzima.

Amesema ipo mikoa ambayo wameshaenda tayari ,kwa Arusha wameanza zoezi hilo 7sept 2020 na litafanyika katika katika wilaya zote na vitongoji vyake, na watachukua maoni kwa wafanyabiashara,kushughulikia matatizo ya wadau wao na kuwa daraja,pia amewataka kuondokana na ile dhana kwamba TRA ni inatisha au kufunga maduka na kukimbia.

Amesema mambo ambayo wanatolea elimu ya mlipakodi ni pamoja na utunzaji wa kumbukumbu,mauzo kwa siku ,manunuzi na matumizi,hiyo itamrahisishia mlipakodi kupata kodi stahiki wakati anafanyiwa makadiriao, kuliko kukisiwa kwani atajikuta analipa kiasi ambacho sicho chenyewe.

Amesema changamoto kubwa waliyokutananayo katika kuwatembelea wadau hao, ni pamoja na kutokutungika TIN namba zao katika maeneo yao ya biashara,wengine wanasema kuwa zipo nyumbani ama kwenye droo,hawatunzi kumbukumbu.

Kwa upande wake mfanyabiashara aliyepatiwa elimu ta mlipakodi na TRA Winnie Frank ameiomba Mamlaka hiyo kuwaangalia kwani kodi ni kubwa kwa sasa kulingana na kipato wanachokipata kwani biashara ni ngumu na wateja hakuna

Amesema wafanyabiashara wanakwepa na wanafunga maduka kwasababu kodi ni kubwa sana kuliko kile wanachokipata,amewaomba TRA watoze kodi kulingana na kile mfanyabiashara anachokipata itawarahisishia wao kulipa kodi.

Kwa upande wake Robert Tarimo mfanyabiashara wa duka na.360 ameishauri TRA, mara baada ya kupatiwa elimu ya mlipakodi, kwamba kabla ya kuwakadiria kodi ni vyema wakawatembelea ,ili waweze kuwakadiria kulingana na biashara wanazoziendesha.

''Sisi wafanyabiashara tunavyokwenda pale,tunapoongea na wale maofisa pale tunazungumza kulingana na biashara,mara nyingi hawatuamini kwamba biashara ipo kama unavyowaeleza,kwahiyo naomba waje watutembelee kwenye biashara zetu waangalie na yale makadirio''alisema Robert.

  Na. John Mapepele Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Rufiji. Mhe, Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi nch...